Tuesday, 11 September 2012
Watoto 50 kutibiwa moyo India
KLABU ya Lions ya Dar es Salaam, imepanga kuwapeleka nchini India kwa upasuaji wa moyo watoto 50 wanaosumbuliwa na maradhi hayo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa harambee ya kuchangisha fedha za kuwapeleka wagonjwa hao, Mwenyekiti wa hospitali ya Regency, Dk. Rajni Kanabar, alisema watafanya hivyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Lions Club duniani.
“Hivi sasa kuna wagonjwa wa moyo 300 wako kwenye orodha ya kusubiri, na sisi hatuna uwezo mkubwa wa fedha wa kuwapeleka ndiyo sababu tunawaomba wafadhili kutoka makampuni na watu mbalimbali kuchangia watoto hawa waende kupata tiba”, alisema.
Katibu wa klabu hiyo, Mathew Alex, alisema wameamua kuomba msaada kwa Watanzania mbalimbali ili watoto hao wenye matatizo ya moyo waende India kwa matibabu.
“Kaulimbiu yetu ni ‘Miss a Meal to save a Child’, tunaomba mtu akose mlo mmoja ili aokoe maisha ya mtoto mmoja,” alisema Alex.
Alisema takwimu zinaonyesha kwamba zaidi ya watoto 8,000 wanazaliwa na matatizo ya moyo kila mwaka na asilimia 10 tu ndio hupata matibabu sahihi kwa muda na kupona.
“Tunaamini kwamba kila Mtanzania akihamasika kutoa shilingi elfu moja kwa idadi yetu watu zaidi ya milioni 40 tunaweza kukusanya zaidi ya bilioni 40 na kusaidia kupeleka nje zaidi ya watoto 50 kwa matibabu,” alisema.
Mwenyekiti wa kundi la makampuni ya Saibaba, Nathumal Sajnani, alisema kilele cha kampeni hiyo ya uchangishaji fedha itakuwa Oktoba 8.
Alisema watoto hao watakwenda kutibiwa katika Hospitali ya Narayana Hrudayalaya iliyoko mji wa Bangalore na ile ya Fortis Escorts iliyoko New Delhi ambazo zimepunguza gharama za upasuaji kuwa dola 2,000 kwa mgonjwa.
Rais wa Klabu ya Lions, Nimira Gangji, alimshukuru Rais wa Satya Sai Society ya Dar es Salaam ambayo imeahidi kugharamia matibabu ya watoto 15 na Shirika la Emirates kwa kutoa punguzo la nauli za ndege kwa asilimia 25.
Gangji alishukuru Ubalozi wa India kwa kutoa visa bure, Wizara ya Afya Zanzibar na wafadhili mbalimbali ambao hawakutaka majina yao yatajwe.
Msamaria mwema anayeguswa kuwachangia watoto hawa, atume fedha kwenye simu 0768 – 620805, M- pesa: 0652 – 620808 na 0688 – 477969
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment