WELCOME TO VIBES,FEEL FREE AND ENJOOY

Tuesday, 11 September 2012

KITENGE NA KHANGA KUWA VAZI LA TAIFA

Kitenge na Khanga vimeteuliwa rasmi kuwa vazi la Taifa ambapo litaanza kuvaliwa rasmi katika sherehe za miaka 51 ya uhuru wa Tanzania zitakazoadhimishwa Desemba 9 mwaka huu. Khanga na Vitenge hivyo vitakuwa katika sura inayotambulisha utamaduni halisi wa tanzania ambapo baadhi ya alama zitakazoshamiri katika vazi hilo ni bendera ya Tanzania, wanyama, ngoma, mwenge wa uhuru, ngao, ala za muziki wa asili, mlima kilimanjaro pamoja na madini na mazao. Uteuzi huo umefikiwa na kamati iliyoundwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo mwishoni mwa mwaka jana kwa nia ya kuchagua kitambaa ambacho kitakuwa ni vazi la taifa kwa kila mtanzania kulitambua. Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kuwasilisha ripoti inayoonesha michoro ya vazi la taifa litakalokuwa katika mtindo wa Khanga na Kitenge, Katibu wa kamati hiyo Angel Ngowi alisema zoezi la kusaka kitambaa cha vazi la taifa lilianza tangu mwaka 2003. Alisema mchakato huo uliwashirikisha watanzania kwa kutoa maoni yao juu ya vazi hilo la taifa liwe na muonekano gani. Alisema ili kufikia malengo hayo waliandaa mashindano ya michoro yaliyoshirikisha jumla ya wasanii 88 ambao waliwasilisha jumla ya michoro 200. Alisema kati ya wasanii hao ni wasanii sita ndio waliokuwa wametimiza vigezo na matwakwa ya vazi la taifa ambapo wasanii hao waliunganishwa na wataalam wa vitambaa kwa ajili ya wakidizaini jinsi vazi hilo litakavyokuwa katika muonekano wa khanga na kitenge.

Alisema wataalam pamoja na wasanii hao walitengeneza michoro mitano yenye muonekano tofauti katika kitenge na michoro minne yenye muonekano tofauti katika khanga ambayo ndiyo iliyowasilishwa jana kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Fenella Mukangara. Kutokana na kazi ya wajumbe hao kukamilika, Waziri Fenella ameishukuru kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Joseph Kusaga kwa kazi ngumu walioifanya. Waziri Fenella ameiagiza menejimenti ya Wizara yake chini ya Usimamizi wa Katibu Mkuu ichague michoro minne kati ya iliyowasilishwa na kamati hiyo ili ipelekwe ngazi ya Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri na Kamati ya Ufundi ya Makatibu wakuu kwa kuipitia. Waziri Fenella alisema mchakato huo anategemea ufikie tamati Oktoba 31 mwaka huu ili viwanda vya nguo vihamasishwe kuzalisha kwa wingi na kwa ubora vitambaa vya Khanga na vitenge vilivyoteuliwa kushonwa kwa vazi hilo la taifa. "Seikali ingependa kuona kwamba wakati tunasherehekea miaka 51 ya Uhuru Desemba 9 mwaka huu kuwepo tayari na vazi hili katika maduka yote ili wananchi washiriki sherehe hizi wakiwa wamevaa vazi la taifa,"alisema Waziri Fenella. Wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo iliyosimamia mchakato mzima wa kupatikana vazi la taifa ni Mustapha Hasanali na Ndesumbuka Merinyo ambao ni wabunifu wa mavazi nchini, Joyce Mwavile, Angel Ngowi pamoja na wajumbe wengine.

No comments:

Post a Comment