WELCOME TO VIBES,FEEL FREE AND ENJOOY

Friday, 16 March 2012

Lowassa atoboa siri ugonjwa wake

WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amerejea nchini kutoka Ujerumani alikokwenda kwa matibabu na kuzungumzia afya yake akisema anasumbuliwa na ugonjwa wa macho,na kujitutumua kwa kukunja ngumi huku akitamba kuwa yuko tayari kwa mapambano.

Tangu mwanasiasa huyo alipondoka nchini kimya kimya wiki kadhaa zilizopita kwenda Ujerumani kwa matibabu, suala la afya yake limezua gumzo na kuibua mijadala kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, huku baadhi ikidai hali ni mbaya.

Machi 7 mwaka huu, Lowassa alilitihibitishia Mwananchi kwamba alikuwa hospitalini nje ya nchi lakini, hakuwa tayari kufafanua alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa gani wala kutaja hospitali aliyolazwa.  

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam, Lowassa alisema alikwenda Ujerumani kuchunguzwa tatizo la macho ambalo lilikuwa likimsumbua.

"Kumekuwa na maneno mengi kuwa naumwa na wengine wakisema ni mgonjwa sana lakini, yote hayo ni uongo,"alisema Lowassa na kuongeza:

"Nilikuwa Ujerumani kwa ajili ya kuchunguzwa macho kama yana matatizo. Profesa wangu aliniambia niende ili kuangalia kama nahitajika kufanyiwa operation (upasuaji) lakini, ameniambia sina tatizo na afya yangu ni nzuri na pia mapigo yangu ya moyo yako 120/40 niko vizuri na sina presha."

Lowassa alisema alichokuwa akikifanya huko ni kuangalia afya yake, na kuwaomba watu wajue kuwa hana tatizo lolote.

Katika kuthibitisha kwamba hana tatizo lolote, Lowassa alikunja ngumi mbele ya waandishi wa habari na kunyosha mikono yake huku akicheka , kuthibitisha kuwa yu buheri wa afya.

Alifanya hivyo baada ya kuombwa na mmoja wa waandishi wa habari athibitishe kama yuko mzima wa afya. "Niko vizuri, niko tayari kwa mapambano yaliyoko mbele yetu," alisema Lowassa bila kufafanua ni mapambano gani.


Ingawa hakutaka kufafanua mapambano yake hayo, Lowassa amekuwa akitajwa kutaka kuwania urais mwaka 2015, kumrithi Rais Jakaya Kikwete atakapomaliza muda wake kikatiba.

Lowassa alikataa kujibu maswali mengine ikiwemo kampeni za ubunge Arumeru Mashariki kwa mgombea wa CCM, Sioi Sumari kuhusishwa na yeye.

Alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa  mkutano huo ulikuwa maalumu kuzungumzia suala la afya yake.

Regina Lowassa

Kwa upande wa mke wake, Regina,  aliyekuwa amefuatana naye, alisema mumewe ni mzima na yuko imara kwa kuwa hana tatizo lolote.

"Mume wangu hajambo, yuko imara kabisa na hana tatizo lolote,"alisema Regina.

Hata hivyo, mkutano huo ulikuwa na mazingira magumu kwa waandishi wa habari kuuliza maswali mengine baada ya baadhi ya wenzao kuwazui. 
"Mheshimiwa alitaka kuzungumzia tu afya yake na si kitu kingine."Zilizikika baadhi ya kauli zikisisitiza.

Utata wa afya yake

Wakati Lowassa anazungumza na gazeti hili Machi 7 mwaka huu, alijibu kama ifuatavyo:

Swali: Asalaam alaykum Mheshimiwa Lowassa.
Jibu: Waalaykum Salaam.

Swali: Mimi naitwa... (jina la mwandishi) kutoka gazeti la Mwananchi. Kwanza pole kwa matatizo ya kiafya yanayokusumbua.
Jibu: Ahsante.

Swali: Nimekupigia pamoja na kukupa pole, nilitaka kujua unaendeleaje na matibabu?
Jibu: Niko hospitalini kwa sasa naomba niache mambo mengine tutaongea baadaye.

Swali: Lakini, ni matibabu gani hasa unayopata?
Jibu: ... (akimtaja mwandishi) naomba niache niko hospitalini sasa hivi mambo mengine tuongee baadaye. 

Lowassa alitoa majibu hayo majira ya saa nane mchana na alipopigiwa tena saa 10.20 jioni, alijibu kama ifuatavyo:

Swali: Naam, Mheshimiwa Lowassa nimekupigia tena mimi... (mwandishi akajitambulisha). 
Jibu: ... Unataka nikuambie nini tena? Nilishakwambia niko hospitalini niache!

Swali: Sawa, natambua uko hospitalini, lakini wewe ni kiongozi ambaye umewahi kuwa Waziri Mkuu, hivyo Watanzania wangependa kujua maendeleo ya afya yako kutokana na utata ulioibuka na kama je, umelazwa hapo hospitalini au uko katika matibabu ya kawaida?
Jibu Niache, ninachokwambia niko hospitalini sasa unataka nini tena? Nisingependa kuzungumzia afya yangu kwa undani. 
CHANZO:-MWANANCHI 

No comments:

Post a Comment